ASASH GENERAL TRADERS

ASASH GENERAL TRADERS

Thursday, February 6, 2014

WAAMUZI WANAKOSEA KATIKA MECHI ZA TIMU KUBWA TU??



Baraka Mbolembole

WAAMUZI, hivi sasa wamekuwa kero kubwa kwa wapenzi wa soka nchini kutokana na kuboronga kwao katika michezo mbalimbali ya ligi kuu inayoendelea nchini. Abdallah Kambuzi, mwamuzi huyu alichezesha mchezo kati ya Yanga SC na Mbeya City, jumamosi iliyopita alionekana kushindwa kufanya maamuzi sahihi. Si yeye tu kumeibuka malalamiko zaidi kutoka kwa timu nyingine kuhusu uchezeshaji mbaya wa waamuzi wengi nchi.

Nao ni binadamu, hivyo kufanya makosa ni jambo la kawaida. Kama mchezaji hufanya makosa na kuadhibiwa, hivyo mwamuzi nae anaweza kufanya makosa. Ila pamoja na adhabu mbalimbali ambazo wamekuwa wakipata bado hali si nzuri. Wamekuwa wakifanya makosa  kwenye mechi za Yanga, Simba na Azam FC, tena ni makosa ya makusudi kabisa. Mfano, ni kadi nyekundu ambayo alipewa kiungo wa City, Steven Mazanda wiki iliyopita katika mchezo dhidi ya Yanga, na matukio ambayo yalifanywa na Haruna Niyonzima, baada ya kiungo huyo wa Yanga kuwa na kadi ya njano, baadae alitakiwa kuondoshwa uwanjani kwa kadi ya pili ya njano ila haikuwa hivyo, mwamuzi akaamua kukataa bao lililokuwa halali la Hamis Kizza kama  njia ya kusahihisha makosa yake.

WANAPANGA MATOKEO?

Bado hakuna ushahidi wa moja kwa moja kuhusu hilo, ila  timu nyingi zimekuwa zikiandaa 'fungu' la marefa ili wapate upendelo. Katika mchezo wa Ntibwa Sugar na Simba, kocha wa Mtibwa, Mecky Mexime alionekana kuwa na jabza kuhusu uamuzi wa mwamuzi , Deonisia Kyura ambaye alimtoa nje kiungo na nahodha wa timu yake Shaaban Nditti. Awali Nditti alikuwa na kadi ya njano ila aliamua kumchapa kofi Amis Tambwe ambaye alimbana na miguu walipokuwa wameanguka wote chini.

Nditti, inadaiwa alitoa lugha chafu kwa mwamuzi huyo ndiyo maana akaadhibiwa, ila muda mwingi alionekana kushindwa kuendana na ukubwa wa mechi. Kwa nini alipangwa? Tafakari....
Bahati mbaya ni kuwa waamuzi hao wamekuwa wakilalamikiwa zaidi katika michezo dhidi ya timu kubwa tu, huku wanapokuwa wakichezesha michezo dhidi ya timu nyingine nje ya Yanga, Simba na Azam wamekuwa wakifanya vizuri. 
WANACHEZESHA KWA KUFUATA MAELEKEZO...
Ndiyo ukweli ulivyo, ila ni vigumu mtu wa Yanga, Simba au Azam kusema kuwa wanakuwa wakipata ' mbereko' kutoka kwa waamuzi. Tatizo hili linajulikana na wahusika ni viongozi wa klabu, waamuzi na wasimamizi wao. Klabu ndiyo zimekuwa zikihusika moja kwa moja kwa nia ya kupata matokeo ya ushindi tu. Mambo haya yanakera. Waamuzi nao ni binadamu hivyo ni rahisi kuingia katika ushawishi wa kuchukua pesa zinazowekwa mezani na viongozi wa klabu.
Mambo haya naamini yanafahimika kwa wahusika hivyo wanatakiwa kuchukua hatua ya haraka ya kuachana na mambo hayo ili kufanya timu zetu zishinde kwa uwezo wao, na mwisho tupate mabingwa sahihi. Siku zaidi ya 100 za rais wa TFF, Jamal Malinzi, soka la Tanzania bado lipo majaribuni. Waamuzi ni changamoto nyingine kubwa kwake. Awakataze kuchezesha kwa maagizo kutoka nje ya uwanja.

No comments:

Post a Comment