Na Othman Khamis Ame, OMPR
Kocha Mkuu wa Italy Cesare Psandell ameishauri Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo kuandaa mpango maalum utakaomuewezesha kusaidia kuinua kiwango cha mchezo wa Soka hapa Nchini.
Kocha Cesare ameamua kusaidia kukuza kiwango cha soka cha Zanzibar kufuatia ukarimu wa watu wake pamoja na mazingira mazuri yaliyopo ndani ya Visiwa vya Zanzibar unaoleta ushawishi wa watalii na wageni wengi kupendelea kutembelea Visiwa hivi.
Gwigi huyo wa Taaluma ya kufundisha Soka Nchini Italy alieleza hayo wakati akibadilishana mawazo na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo Ofisini kwake Mtaa wa Vuga Mjini Zanzibar.
Kocha Cesare alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba angependelea kuona Zanzibar inamjengea mazingira ya chuo maalum cha soka atakachoweza kufundisha wakati anapokuja mapumziko ya kila mwaka hapa Zanzibar.
“ Nimeamua kuisaidia Zanzibar kisoka kwa vile muda wangu wa mapumziko ya mwaka karibu mwaka wa tatu sasa nautumia hapa Zanzibar. Sasa ingekuwa ni jambo la msingi na busara muda huo nikatumia taaluma yangu kwa vijana wangu wa hapa Zanzibar. Najihesabu kwamba Zanzibar ni makazi yangu ya pili katika maisha yangu ukiachilia Italy “. Alifafanua Kocha Mkuu huyo wa Soka Nchini Italy.
Alieleza kwamba wakati umefika kwa chama cha soka cha Zanzibar { ZFA } kikaanza kufanya mawasiliano ya ushirikiano na shirikisho la soka Nchini Italy ili kutoa fursa itakayomjengea njia muwafaka ya kuanza kusaidia kufundisha soka hapa Zanzibar.
Kocha Cesare alihafamisha kwamba mawasiliano hayo kwa njia moja ni mwanzo wa kuongeza uhusiano wa karibu zaidi kati ya wananchi na jamii za Zanzibar na wenzao wa Italy.
Alieleza kwamba Zanzibar kwa kiasi kikubwa imekua kiuwezeshaji ikilinganishwa na mataifa mbali mbali ulimwenguni jambo ambalo limesaidia wawekezaji wengi nje ya nchi kushawishika kutaka kuwekeza vitega uchumi vyao ndani ya Visiwa vya Zanzibar.
Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko tayari kushirikiana na Kocha Mkuu huyo wa Italty katika azma yake ya kutaka kusaidia kunyanyua kiwango cha mchezo wa Soka hapa Zanzibar.
Balozi Seif alisema Kocha Cesare Pzandell yuko huru wakati wowote ule kusaidia, kushauri au kuelekeza masuala yoyote yanayohusu fani yake ya mchezo wa soka ili utaalamu wake uweze kusaidia wanamichezo hapa Nchini.
“ Kwa kuwa uwepo wako nchini utasaidia kunyanyua kiwango cha soka Zanzibar uko huru kutusaidia katika kutushauri na kutuelekeza katika muelekeo wa kunyanyua kiwango chetu cha soka hapa Nchini “. Balozi Seif alimfungulia milango wazi kocha huyo wa Italy Cesare.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliiagiza Wizara ya Habari, Utamduni, Utalii na Michezo kujipanga vyema katika utaratibu wa kumuandalia mpango maalum utakaomuwezesha kocha huyo kuanza kutoa taaluma ya soka hapa nchini.
Mapema Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamduni, Utalii na Michezo Dr. Ali Saleh Mwinyikai alisema Kocha Mkuu wa Soka wa Italy Cesare Pzandell tayari ameshaonyesha nia ya kujenga uhusiano mzuri na wakaribu na Zanzibar katika masuala ya soka na kusema kwamba atafarajika zaidi atakapoona Zanzibar katika siku chache zijazo inapanda chati katika medani ya Soka Duniani
No comments:
Post a Comment