ASASH GENERAL TRADERS

ASASH GENERAL TRADERS

Tuesday, February 3, 2015

KABURU AWAPINGA WANAOMUONESHEA KIDOLE


MAKAMU wa Rais wa Simba, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’, ameibuka na kueleza kinachoitafuna klabu hiyo na kujikuta ikisuasua kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara, akisisitiza kuwa yeye si tatizo kama inavyovumishwa na baadhi ya adui zao.
 Kaburu alisema kila kitu ndani ya Simba kipo sawa pamoja na kuwepo taarifa kuwa hana uhusiano mzuri na mmoja wa viongozi wenzake wa Kamati ya Utendaji, akiwemo Rais wa timu, Evans Aveva.
 Kaburu aliliambia BINGWA kikosi cha Simba hivi sasa kinakabiliwa na changamoto nyingi kwenye ushiriki wao wa Ligi Kuu Tanzania Bara ambapo alizitaja changamoto hizo kuwa ni wachezaji wengi kuwa vijana, ubovu wa viwanja na ukosaji umakini wa waamuzi.
 Aliongeza kutokana na changamoto hizo, ikitokea timu imepata matokeo mabaya, baadhi ya viongozi wamekuwa na tabia ya kutafuta mchawi kitu ambacho si sahihi.
 Alisema mpira una matokeo matatu; kushinda, kufungwa au sare na kwamba inapotokea timu inafanya vibaya, haina maana imehujumiwa, ni matokeo ya uwanjani hivyo si vyema kuanza kushikana uchawi.
 “Kwa sasa nimekomaa kwenye uongozi, mnapokuwa mnaongoza kitu au taasisi fulani, kuna kipindi maneno mbalimbali yanaibuka, sina sababu kupigizana kelele na mtu, siku zote ukiwa kiongozi lazima ukubali kupingwa na kukubaliwa,” aliongeza Kaburu.
 Alisisitiza kiongozi mzuri siku zote ni yule anayekubali kukosolewa, kutokana na hilo, ameamua kujipanga kukabiliana na changamoto zilizopo ndani ya klabu hiyo.
 Alisisitiza mbali na changamoto hiyo, Simba ina changamoto nyingine ya kocha kwani aliyepo sasa, Mserbia Goran Kopunovic, hana uzoefu na soka la hapa nchini, hivyo kumwia vigumu kuzoea haraka mazingira ya maisha ya soka la Tanzania.
 “Mbali na changamoto ya kuwa na wachezaji wengi vijana, kocha mpya na nyinginezo,  lakini pia hata waamuzi wetu wamekuwa kikwazo kikubwa kupata ushindi, wanashindwa kufuata sheria 17 za mchezo wa soka, hii pia ni changamoto nyingine kwetu,” aliongeza.
 Simba iliyofanikiwa kutwaa ubingwa wa Kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar Desemba mwaka jana, Jumamosi iliyopita iliichapa JKT Ruvu mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, lakini ikiwa ni baada ya kulambwa mabao 2-1 na Mbeya City Jumatano ya wiki iliyopita.

No comments:

Post a Comment