ASASH GENERAL TRADERS

ASASH GENERAL TRADERS

Sunday, February 9, 2014

HII YA MALINZI KIBOKO


Na Baraka Mbolembole
Mabepari wapo kila mahali, pia wana misingi mikubwa ya kifedha, na mahusiano makubwa na vyombo vya umma. Kwa mfano wana uhuru wa kutumia vyombo vya habari. Ila kama kiongozi anakuwa akiwavutia watu, basi ni kwa sababu ni kwa sababu yeye mwenyewe amavitiwa na hiyo kazi iliyo mbele yake. Watu ndiyo nguvu pekee inayoweza kusaidia mabadiliko. Hivyo kiongozi anatakiwa kuwaunganisha watu na kuwafahamisha kwamba umoja wao utasaidia kupata wanachotaka. Ila watu nao wanatakiwa kuamka.

Katika soka la Tanzania,  tunaweza kusema kuwa tumempata mtu ambaye tulikuwa tukimuhitaji, kwani  rais wa sasa wa Shirikisho la Soka Nchini, TFF, Ndugu, Jamal Malinzi  anaijua Jiografia ya Tanzania, na analifahamu vizuri soka la nchi hii.  Hivyo atakuwa anafahamu mahitaji  na mawazo yanayotakiwa ili kukuza mpira wa Tanzania. Malinzi licha ya kutajwa kama kiongozi hodari baada ya kupita kwa zaidi ya siku 100 za utawala wake, ameonesha kuwa muhubiri hodari shupavu, na bila shaka atakuwa mwanafunzi hodari pia. Na hili litawezekana endapo ataamua kutumia muda wake kutazama na kujifunza zaidi kuhusu nini hasa kinachotakiwa kuanza ili kupata msingi imara wa mpira wetu.

Soka mara zote linakuwa na mahitaji ya muda mfupi na muda mrefu. Malinzi ameingia na mipango yake, huku soka la vijana likiwa kipaumbele kikubwa kwake, na hapo Academy za soka anaamini ndiyo suluhisho la kwanza. SAwa ni jambo zuri kwa kuwa ameingia huku akiwa na kiu ya kufanikisha mipango aliyojiwekea. Sera yake kuhusu soka la vijana ni nzuri, na ziara yake aliyoifanya siku za nyuma katika Academy ya Allience Sports ya jijini Mwanza, ilirutubishwa na maneno mazuri kuwa hapo ndiyo kutakuwa kitovu cha mpira wa Tanzania. Hadi sasa Malinzi ameonesha kuwa mtu anayependa sana kazi yake, ila mikakati yake ni lazima iendane na uhimarishaji wa soka la mitaani.

Jiografia ya Tanzania, bado mchezo wa soka unahitaji unahitaji kuwekewa mkazo mkubwa sana katika ngazi za chini, kata, tarafa, wilaya na mikoani, kwa kuwa uchumi wetu hauwezi kuendana na mkakati wa Academy kwa nchi nzima. Vipaji ni vingi sana nchini. Labda huu ni wakati wa kuanzisha ligi za vijana ambazo muendelezo wake utakuwa hadi ngazi ya Kitaifa, kwa kuwa na michuano inayotambulika na si hii ya muda mfupi kama ilivyo Copa Coca Cola. Mfano michuano hiyo ya Copa, inaweza kufanyika kwa kipindi cha mwaka mzima kwa mtindo wa ligi. Ni ghali sana, ila udhamini ambao makampuni yanapewa katika soka la Tanzania unatakiwa kuendana na hali halisi. 

Mitaani, ndipo soka linapotoka. Ndiyo maana WAingereza wanataka kuhamia na kuweka nguvu zao zaidi katika soka la mitaani kuliko lile la mfumo wa Academy. Muundo mzuri wa mfumo wa soka uhusishe pia namna ya kuendeleza vipaji ambavyo kimsingi haviwezi kupata nafasi katika Academy kuwa kuwa mambo ya uchaguzi huendana na ukiritimba mkubwa kila mahali. Uzuri wa Academy ni kwamba vijana watakuzwa na kuendelezwa katika mwendo mzuri wa kinidhamu, kutambua majukumu na kuwajibika, ila siku zote ni lazima tutambue kuwa, kila mtoto huzaliwa na tabia njema, tabia mbaya huja baadae. UNaweza kuzalisha wachezaji 100 bora katika nchini na kujona umefanikiwa sana, ila tabia zao kadri wanavyokuwa wakikua zinakuwa zikibadilika. Soka la Academy ni muhimu, ila soka la mtaani ni tumaini la muda wote kwa mpira wa Tanzania.

Majuzi nilikuwa nikiwasiliana na James Julius,  Mtanzania ambaye yupo nchini Afrika Kusini, akifanya kazi katika Academy ya ' Stars of Africa'. Naye ameanza na mikakati ya kufanya uwekezaji katika soka. Ameomba ekali zaidi ya 20 katika mji wa Mwanza ili kuanza ujenzi wa ' Mandozi Sports Academy', maombi yake hayo anataraji kupata majibu mwezi huu. Huyu ni kijana mdogo tu na tayari ametumia zaidi ya millioni 20 kwa kuanzisha timu nne za vijana, U20, U17, U14, na U12. Mimi alinipatia CD za hiki ninachokisema hapa na nimeona mikakati yake. Hivyo kwa Malinzi, bila shaka tayari ametoa mwamko na matumaini kuwa watu wamemuelewa na tayari wanatumia nguvu zao kusaidia soka la Tanzania

Hapa ni makampuni yanayotakiwa kusaidia katika ili na si kusubiri kujitokeza hapo baadae wakati wakiona kuna matunda ya wao kutangaza biashara zao. Makampuni mengi yamekuwa yakijinifaisha kupitia ufadhili wao katika soka la Tanzania, Hata udhamini wanaoupata timu zetu mbili kubwa kwa sasa hauendani na thamani ya klabu hizo. Simba na Yanga zinawaingia faida kubwa wadhamini wao kuliko kile wanachoingiza wao kutokana na ufadhili au udhamini walionao. Makakati, wa Mandozi, Sports Acacemy, Allience Sports Academy unatakiwa kusapotiwa kwa nguvu na makampuni yaliyopo nchini. Yatafikaje, ni kwa wahusika wenyewe kujitokeza na kuonesha kuwa wapo tayari kufanya kitu kikubwa hivyo wanatakiwa kuyafuata makampuni hayo na kuyaomna yaende kuwasaidia.

  WANAOSEMA TFF IMEJAA, U- SIMBA NA U-YANGA NAWASHANGAA

Hivi ni nani anayeweza kuishi nje ya fikra za Simba na Yanga? Labda kwa yule ambaye si mpenzi wa soka. Wakati mwingine sisi binadamu tunakuwa wanafiki kweli. Nani hajui kuwa Jamali Malinzi amewahi kuwa kiongozi wa juu wa klabu ya Yanga? Nani hajui kuwa Geofrey Nyange Kaburu amewahi kuwa kiongozi wa juu wa klabu ya Simba> Vipi kwa kina Abbas Tarimba, Seif Ahmed, David Mosha, Zacharia Hans Poppe, Clement Sanga, mimi ninafikiri muhimu ni kuwashauri kuwa mpira wa Tanzania unawategemea sana wao hivyo wanatakiwa kufanya kazi zao kutokana kanuni na taratibu zilizopo. Wasiweke mapenzi ya vilabu vyao katika mambo muhimu.

Mimi, wewe, sote tumekuwa na upenzi wa soka. Inategemea tu, wewe utakuwa unaangukia wapi katika mapenzi yako, inaweza kuwa Simba, au Yanga ama timu nyingine yoyote ile. Ndiyo, Malinzi amewavuta watu wengi wa Simba na Yanga katika kamati zake, ila si kwa lengo la kuharibu mpira bali kupanga na kusimamia vuzuri mikakati inayoweza kusogeza soka la Tanzania mbele zaidi. Ni makosa kumuhukumu kwa sasa ila hatutosota kumsema vibaya endapo tunashuhudia kamati zake zikifanya mambo kwa kuvutana kisa mapenzi ya u- Simba na u- Yanga. Kwa sasa tuwasisitize wafanye kazi zao vizuri bila kusukumwa na ushabiki na si kuwahuku kwa makosa yasiyokuwepo. Kama hatuwataki hao, kisa ni Simba na Yanga, mleteni basi Sir Alex Ferguson aje kuwa rais wa TFF, kwa kuwa watu wengi wa soka wanatoka katika mapenzi ya dhati ya Simba na Yanga.

Itakuwa ni makosa makubwa kwa Malinzi, endapo watu aliowaamini na kuwapatia nafasi watamuangusha kisa ushabiki wa klabu zao. Itakuwa ni sawa na muwindaji ambaye aliamua kuchukua mtoto wa Simba na kumpeleka nyumbani kwake. Huyu atakuwa amejipelekea maangamizi yeye mwenyewe na familia yake. Soka la Tanzania halihitaji wafanyakazi wa mapenzi, ila ukweli ulio wazi linawahitaji watu waliopita Simba au Yanga, iwe kiuongozi au kiuchezaji. Mkakati wa Malinzi na soka la Tanzania unahitaji fikra zetu sote. Kulaumu kupo tu kila mahali, ila nasi tutoe ushauri mzuri kwao ili kwenda sambamba na matarajio yanayokusudiwa. Nimewasilisha tu. Karibuni pia Mandozi Sports Academy...

No comments:

Post a Comment