RAGE: UCHAGUZI SIMBA SC UPO PALE PALE, KAMATI NI ILE ILE YA NDUMBARO NA MAAMUZI NI YALE YALE, WAMBURA...
Na Renatus Mahima, DODOMAMWENYEKITI wa Simba SC, Alhaj Ismail Aden Rage amesema kwamba, uchaguzi wa klabu hiyo upo pale pale kama ulivyopangwa Juni 29, mwaka huu kwa sababu si yeye wala Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) mwenye uwezo wa kutengua hilo kwa sasa.Akizungumza mjini Dodoma leo mchana, Rage ambaye pia ni Mbunge wa Tabora Mjini (CCM), amesema kwamba yeye hana mamlaka Kikatiba kwa sasa kubatilisha tarehe ya uchaguzi na TFF pia haiwezi kufanya hivyo.Rage ameungana na Kamati ya Uchaguzi ya klabu hiyo kupinga maamuzi ya Rais wa TFF, Jamal Malinzi kusimamisha mchakato wa uchaguzi mkuu wa klabu hiyo.Rage amesema uchaguzi wa Simba SC upo pale pale kama ilivyopangwa Mwishoni mwa wiki Malinzi alitoa tamko la kusimamisha mchakato wa uchaguzi mkuu wa klabu hiyo uliopangwa kufanyika Juni 29 mwaka huu hadi pale klabu hiyo kongwe nchini itakapounda kamati ya maadili.Akizungumza na waandishi wa habari kwenye Ukumbi wa Idara ya Habari ya Bunge mjini hapa leo mchana Rage amesema amelazimika kumwandikia barua Malinzi ili kuinusuru klabu hiyo iliyokubwana migogoro kwa takriban miaka miwili sasa.“Juni 15 mwaka huu nilipokea barua kutoka kwa Rais wa TFF, Jamal Malinzi akinitaka utekelezaji wa mambo matatu; kwanza kuunda kamati ya maadili, kusimamisha mchakato wa uchaguzi mkuu wa Simba na mwisho kuhakikisha maagizo hayo yawe yamekamilika kufikia Juni 30 mwaka huu,” amesema Rage.“Klabu ya Simba ni muhimu sana katika maisha yangu, nimeichezea na kuitumikia kama katibu mkuu 1982 na nimeingia katika kumbukumbu muhimu kwa kuwa Rais wa kwanza wa klabu hii.“Kwa kutambua hilo, leo nimemwandikia barua Malinzi kumwomba asisitishe uchaguzi wetu, aache ufanyike Juni 29 kama iilivyopangwa. Ninatambua anayo mamlaka ya kuweza kuuchelewesha.“Usajili umeanza tangu Juni 15 mwaka huu, kusitisha uchaguzi ni kutoitendea haki klabu ya Simba kwa sababu mimi na uongozi wote unaomaliza muda wake tumezuia usajili hadi pale viongozi wapya watakapopatikana,” amesema zaidi Rage.Kuhusu kuunda kamati ya maadili, Rage amesema masuala mengi ya kimaadili yanayowakabili baadhi ya wagombea akiwamo Michael Wambura aliyeenguliwa katika kinyang’anyiro cha Urais, yako juu ya uwezo wa klabu ya Simba, hivyo anayarudisha TFF.“Masuala mengi ya kimaadili ambayo Rais wa TFF ametaka yaundiwe kamati ya maadili ya klabu ili yasikilizwe yako juu ya uwezo wa Simba,” amesema Rage.“Wambura anakabiliwa na makosa ya enzi za FAT (Chama cha Soka Tanzania – sasa TFF), Simba haina mamlaka ya kuyasikiliza, hivyo nimeyarudisha kwa Malinzi kule TFF,” amesema Rage.Lakini, licha ya Rage kuandika barua kwa Malinzi, tayari Kamati ya Uchaguzi ya Simba imetoa tamko kwamba haitasimamisha mchakato wa uchaguzi kwa vile Rais huyo wa TFF hana mamlaka kikatiba kuizuia kuendelea na mchakato huo.Aidha, Rage alitumia mkutano huo kukanusha taarifa zilizotolewa na vyombo vya habari leo kuwa ameivunja Kamati ya Uchaguzi ya Simba inayoongozwa na Damas Ndumbaro ambayew ni daktari wa sheria.“Sijaivunja Kamati ya Uchaguzi ya Simba kwa sababu sina mamlaka ya kuivunja kikatiba na sijaongea na chombo chochote cha habari kuhusu hili,” amesema Rage.
No comments:
Post a Comment