ASASH GENERAL TRADERS

ASASH GENERAL TRADERS

Monday, December 16, 2013

OKWI SIO WA SIMBA TENA!


MSHAMBULIAJI mpya wa Yanga, Emmanuel Okwi ametua nchini leo mchana tayari kwa kuitumikia klabu yake aliyoingia nayo mkataba hivi karibuni.

Okwi ametua nchini akitokea kwao Uganda kwa ndege ya Shirika la Ndege la Kenya maarufu kama KQ na kulakiwa na baadhi ya viongozi wa Yanga.

Kwa mujibu wa viongozi wa Yanga, Okwi anatarajiwa kuanza mazoezi na Yanga muda wowote kuanzia sasa na hata kesho asubuhi anaweza kuwepo katika mazoezi ya timu hiyo kwenye Uwanja wa Bora, Kijitonyama.

Okwi amejiunga na Yanga kwa mkataba wa miezi 30 akitokea SC Villa ya Uganda ambayo ilimchukua mchezaji huyo kutoka Etoile du Sahel ya Tunisia baada ya klabu hiyo kushindwa kumlipa stahiki zake.

Ingawa hati ya uhamisho wa kimataifa (ITC) ya Okwi imeshatumwa nchini, bado hali ya mambo inaweza kuwa tofauti kwani viongozi wa Simba wanaonekana kutokubaliana na uhamisho huo wa Okwi kwani ‘bado’ wanaidai Sahel.

Suala hilo la madai ya Simba kwa Sahel limefika kwa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) ambalo lilimthibitisha kuichezea Villa kwa hali maalum.

Naam, Okwi ameshatua katika kikosi cha Yanga na tusubiri tuone kitakachotokea japokuwa inafahamika wazi kwamba Yanga imeshamalizana na Villa juu ya kumtumia mchezaji huyo.

 

 

OKWI KUKABADILI KIKOSI CHA YANGA

MUDA mfupi tu baada ya Yanga kukamilisha usajili wa straika wa zamani wa Simba, Emmanuel Okwi kutoka SC Villa, moja kwa moja mchezaji huyo anaingia katika kikosi cha kwanza na kutibua mambo kibao yalivyokuwa awali.

Kabla ya Okwi kutua Yanga, kikosi cha kwanza cha klabu hiyo kilikuwa kinaundwa na Ali Mustapha ‘Barthez’, Mbuyu Twite, David Luhende, Kelvin Yondani, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Athuman Idd ‘Chuji’, Haruna Niyonzima, Frank Domayo, Didier Kavumbagu, Hamis Kiiza, Mrisho Ngassa.

Kwa vyovyote vile, Okwi ni lazima acheze katika kikosi cha timu hiyo hivyo Kocha Ernie Brandts ana kazi ya muhimu kuhakikisha ana-adjust kikosi chake ili kumpatia nafasi Okwi.

Kutokana na ukweli kwamba, Okwi anaweza kucheza kama namba tisa pia, ni wazi mmoja kati ya Kavumbagu au Kiiza anatakiwa aanzie benchi ili kumpisha Okwi ambaye anaweza kuwa mchezaji staa ndani ya kikosi cha Yanga ukimtoa Niyonzima.

Mtandao huu ulipozungumza na Brandts kuhusu hali hiyo, alisema kimsingi Okwi ni mchezaji kama wachezaji wengine na kinachotakiwa sasa ni kila mchezaji kujituma ili kujihakikishia nafasi kikosini.

“Nafurahi timu yetu kumpata Okwi, wanachotakiwa kama wachezaji ni kujituma ili kuhakikisha timu inapata ushindi,” alisema Brandts ambaye ni raia wa Uholanzi.

Wachezaji kadhaa wa Yanga wamefurahishwa na ujio wa Okwi katika kikosi chao na wamesema watahakikisha wanasaidiana naye kuhakikisha timu inafanya vizuri.

Okwi amejiunga na Yanga akitokea SC Villa ya Uganda ambapo amesaini mkataba wa miaka miwili na nusu kuichezea timu hiyo. Mchezaji huyo anatarajiwa kuwasili Tanzania keshokutwa Jumatano.

No comments:

Post a Comment