ASASH GENERAL TRADERS

ASASH GENERAL TRADERS

Friday, October 3, 2014

KILIMANJARO YAZINDUA NANI MTANI JEMBE 2

1 Dar es Salaam: Awamu ya pili ya kampeni ya Nani Mtani Jembe imezinduliwa leo kwa waandishi wa habari na itazinduliwa kwa wadau wa Simba na Yanga kesho tarehe 4 Oktoba 2014 katika viwanja vya Leaders Club jijini Dar es salaam na itajulikana kama Nani Mtani Jembe 2.
Akiongea katika mkutano na waandishi leo, George Kavishe, Meneja wa bia ya Kilimanjaro Premium Lager, alisema, “Dhumuni la kampeni yetu ya pili ya Nani Mtani Jembe ni kuisogeza Kilimanjaro Premium Lager karibu na wateja wake na wananchi na kuhamasisha ushindani kati ya mashabiki wa Simba na Yanga kwa kushindanisha mamilioni ya mashabiki wa klabu hizi nchi nzima kwa kipindi cha wiki kumi kuanzia Oktoba hadi Disemba.
Alisema, “kampeni hii itazinduliwa na mlolongo wa matukio ambapo tukio la pili litakuwa ni uzinduzi rasmi kwa wadau jijini Dar es salaam ambapo Nani Mtani Jembe 2 itatambulishwa kwa wadau na mashabiki wa Simba na Yanga. Uzinduzi huu utafuatiwa na hafla fupi za kuzindua kampeni hii katika viwanda vyote vya bia ya TBL nchini katika mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya, Moshi na Arusha lengo likiwa ni kuongeza uelewa wa wafanyakazi wa TBL kuhusu Nani Mtani Jembe 2 ili waweze kuwa mabalozi wazuri. Pamoja na kampeni hiyo, tutakuwa na uzinduzi wa kipindi cha televisheni kiitwacho “Kili Chat ”ambacho kitarushwa hewani kwa muda wa wiki kumi kikijumuisha watu maarufu nchini ili kuitangaza Nani Mtani Jembe 2 zaidi na kuhakikisha uwanja wa Taifa unajaa siku ya mechi. ”
2
Akieleza utaratibu wa kampeni hiyo, Kavishe alisema kampeni hiyo itahusisha mashabiki wa Simba na Yanga ambapo jumla ya shilingi milioni 100 zitatolewa na kugawanywa kama ifuatavyo;
a) Shilingi milioni 20 itakuwa zawadi ya fedha kwa ajili ya mechi ya Nani Mtani Jembe 2, ambapo timu itakayoshinda itaondoka na kitita cha shillingi milioni 15 na shillingi milioni 5 zitatolewa kwa timu itakayofungwa mechi.
b) Kampeni hiyo itaendeshwa kwa njia ya sms ambapo mashabiki watapiga kura kwa njia ya sms na shilingi milioni 80 zitagawanywa kati ya timu hizo mbili. Kwa hiyo kila timu itaanza na shillingi milioni 40 kwenye benki maalum mtandaoni kwa ajili ya shindano.
Kavishe alisema kwa kila bia ya Kilimanjaro Premium Lager yenye ujazo wa 500ml mnunuzi atakuta namba maalum chini ya kizibo cha bia hiyo, namba hizo atazitumia kutuma sms kwenda kwenye namba maalum 15415.
Alendelea kusema kuwa ni lazima mnunuzi aandike kwenye sms kuwa yeye ni shabiki wa timu ipi kwa kuandika neno SIMBA au YANGA ikifuatiwa na namba zilizopo chini ya kizibo, na anapotuma sms ataweza kupunguza shilling 10,000 kwenye benki ya timu pinzani na kuweka kiasi hicho kwenye timu yake.
Mwisho wa kampeni hiyo kila klabu itakuwa imeongeza au kupoteza kiasi cha fedha kwa timu pinzani, kulingana na jinsi mashabiki walivyopiga kura.
3
Alisema, “kwa mfano, kama mashabiki wa Simba watapiga kura zaidi ya mashabiki wa Yanga itamaanisha kwamba Simba itashinda na kupata fedha zaidi kutoka kwenye kiasi cha milioni 80, hivyo hivyo kwa mashabiki wa Yanga kama watapiga kura zaidi kuliko mashabiki wa Simba itamaanisha Yanga itapata fedha zaidi ”
Kampeni hii inatarajiwa kuongeza chachu ya ushindani kati ya mashabiki wa Simba na Yanga kwa kuwapa fursa mashabiki kuonyesha mapenzi yao kwa timu zao. Kampeni hii itafungua mlango kwa Kili kuendelea kuwa karibu zaidi na mashabiki na vilevile itazisaidia klabu hizi kuongeza idadi ya mashabiki na kuimarisha ushabiki na mapenzi kwa timu zao.
Mbali na kampeni ya sms, Nani Mtani Jembe 2 itahusisha mashabiki wa klabu za Simba na Yanga katika promosheni mbalimbali na kuwawezesha kushinda zawadi mbalimbali kila wiki pamoja na fedha taslimu. Kampeni hii itafika kileleni mwezi Disemba ambapo itahitimishwa na mechi ya Nani Mtani Jembe 2 kati ya Simba na Yanga katika uwanja wa taifa jijini Dar es salaam mbele ya mashabiki wa timu hizo. IIi timu ziweze kujiandaa vizuri, kila timu itapata kiasi cha shilingi milioni 30 kwa ajili ya maadalizi ya mechi hiyo zikiwa ni ongezeko kutoka shilingi milioni 20 za mwaja jana.
 

No comments:

Post a Comment